AZAKI Tanzania: Wasichana wanaopata ujauzito shuleni si wahalifu wanaostahili kukatishwa ndoto zao
AZAKI Tanzania: Wasichana wanaopata ujauzito shuleni si wahalifu wanaostahili kukatishwa ndoto zaoLeo (29.06.2017) Asasi za Kiraia nchini Tanzania zimetoa Tamko la pamoja
kuhusu kuwapa fursa wasichana kurudi shuleni baada ya kujifungua.
Kwa Ufupi:
Sisi asasi za kiraia nchini Tanzania leo tumeungana kwa pamoja
kuzungumzia umuhimu wa kuwapa watoto wa kike fursa ya kurudi shuleni
baada ya kujifungua. Nia yetu ni kuona wasichana wakipata fursa
zitakazowawezesha kufikia ndoto zao na kuwa na maisha bora. Kwa mujibu
wa Sensa ya mwaka 2012 asilimia 51 ya watanzania ni wanawake na
wasichana. Chochote kinachowaathiri kundi hili kinaliathiri taifa zima.
Wananchi wanasemaje?
Kwa mujibu wa utafiti wa Sauti za Wananchi (2016) asilimia 71 ya
watanzania wanasema wasichana wapewe fursa ya kurudi shuleni kuendelea
na masomo baada ya kujifungua. Ikumbukwe kwamba elimu katika shule za
umma hugharamiwa na kodi za wananchi ambao ndio waliotoa maoni hayo.
Sera zetu, ahadi zetu na viongozi wetu wanasemaje?
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kilichopewa dhamana ya kuliongoza taifa
letu inatamka wazi kwamba wasichana waliopata mimba watapewa fursa ya
kurudi shuleni baada ya kujifungua.
Vile vile tunatambua kwamba Serikali ilikua na dhamira ya kuona
wasichana hawa wanapata haki ya kuendelea na masomo. Sisi AZAKI
tulishirikiana na Serikali katika mchakato wa kutengeneza sera na
miongozo itakayowawezesha wasichana hawa kuendelea na masomo katika
utaratibu rasmi. Hivyo basi tunaomba nia hii njema iendelee.
Sheria zetu zinasemaje?
Chini ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria nyingine za nchi yetu
mtoto anatambulika kama mtu yeyote mwenye chini ya umri wa miaka 18.
Sheria hizi zinatoa haki ya watoto wote kupata elimu bila ubaguzi wa
aina yeyote ikiwemo ujauzito. Na ikumbukwe Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoongozwa kwa misingi ya sheria.
Wasichana wanasemaje?
Si kweli kwamba wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni ni wahalifu
wanaostahili adhabu ya kukatishwa ndoto zao. Wengi wao hawana elimu
sahihi juu ya haki na wajibu wao na ni wahanga wa matukio ya ubakaji.
Sheria zetu zimetamka wazi kwamba kushiriki tendo la ngono na mtoto
chini ya miaka 18 ni ubakaji. Tafiti zinaonesha kwamba wasichana watatu
kati ya kumi walishiriki tendo la ngono kwa mara ya kwanza bila ridhaa
yao. (UNICEF, CDC and MUHAS, 2009) zaidi ya nusu ya wasichana hao
walisema wahusika waliotekeleza ubakaji huo ni watu wenye nguvu
kuwazidi; ambapo asilimia 32 ni majirani, asilimia 15 ni wenye mamlaka
juu yao na asilimia 7 ni ndugu zao.
Jamii inafaidakaje?
Akina mama walioelimika wana nafasi kubwa ya kujenga jamii endelevu.
Takwimu zinaonesha akina mama walioelimika hujifungulia katika vituo vya
afya kwa msaada wa watalaam jambo ambalo hupunguza vifo vinavyotokana
na uzazi ukilinganisha na wale wasio na elimu. Vile vile utafiti wa
Uwezo (2015) unaonesha kuwa watoto ambao mama zao wana elimu wanafanya
vizuri kwenye masomo kuliko wale ambao mama zao hawana elimu.
Majirani zetu wanasemaje?
Nchi jirani ikiwemo Kenya wana sera na miongozo inayowawezesha wasichana
kurudi shuleni baada ya kujifungua hivyo tunaweza kujifunza kutoka
kwao. Visiwani Zanzibar,tangu mwaka 2010 wasichana wanaopata ujauzito
wanawezeshwa kurudi shule kwa utaratibu maalum kama mkakati wa kupunguza
idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo. Katika nchi zinazotekeleza sera
hii hakuna ushahidi wa kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaopata
ujauzito kwa sababu ya kusoma pamoja na wasichana waliojifungua.Visiwani
Zanzibar kiwango cha wasichana wanaopata mimba za utotoni ni asilimia 8
tu ukilinganisha na asilimia 27 Tanzania Bara (Tanzania Health and
Demographic Survey 2015-6).
Sisi tunasemaje?
Tunatambua kwamba, serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati na thabiti
kabisa ya kuleta maendeleo katika Taifa letu kwa kutoa fursa sawa za
elimu kwa watoto wa Kitanzania pasipo ubaguzi; na isingependa kuona
lengo hili halitimii. Tunaomba waliangalie jambo hili upya na
kulitafutia ufumbuzi.
Na kwa hitimisho, tunaomba mijadala juu ya suala hili isizuiliwe.
Tunaamini watafiti, vyombo vya habari, viongozi wa dini na watanzania
kwa ujumla wana maoni yanayohitaji kusikilizwa. Masuala yenye maslahi ya
kitaifa yanahitaji mjadala wa kitaifa ili kuleta tija kwa Taifa.
===========
Baadhi ya Takwimu zinazotokana na tafiti mbalimbali kuhusu suala hili:
1. Afya ya mtoto inategemea sana na elimu ya mama
38% ya watoto (chini ya miaka 5) wenye mama asiye na elimu walipelekwa hospitali ndani ya siku 1 baada ya kupata homa ukilinganisha na 64% ya wale wenye mama mwenye elimu ya sekondari au zaidi.
2. Ufaulu wa watoto shuleni unategemea sana na kiwango cha elimu cha mama
Katika Utafiti wa Uwezo unaoangalia uwezo wa kujifunza wa watoto wa darasa la 1-3 iligundulika kuwa watoto wenye mama mwenye elimu walifaulu zaidi ya wale wenye mama asiye na elimu na ufaulu uliongezeka kulingana na kiwango cha elimu cha mama.
3. Watanzania wanataka wanafunzi wanaopata mimba warejee shuleni baada ya kujifungua
Katika utafiti wa Sauti za Wananchi wa 2016, 71% ya watanzania wanasema wasichana wapewe fursa ya kurudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
4. Watoto hawa wanafanyiwa vitendo hivyo(ngono) na watu wenye nguvu kuwazidi na ni watu wa karibu
32% wanasema walifanyiwa na Jirani, 32% na mtu wasiyemjua, 7% na ndugu zao.
5. Asilimia ndogo sana ya watoto wanasoma shule za Serikali.
No comments:
Post a Comment