Diamond azuiwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere nchini Tanzania kwa kukosa kibali cha BASATA
Diamond azuiwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere nchini Tanzania kwa kukosa kibali cha BASATA
Mwanamuziki nyota nchini Tanzania, Diamond Platnumz na msafara wake walikuwa katika hali ya taharuki kwa saa kadhaa baada ya kuzuiwa na Baraza la sanaa nchini Tanzania, BASATA walipokuwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenda kutumbuiza nje ya nchi kwa kuwa hakuwa na idhini (kibali ) cha Baraza hilo.
Akizungumza na Shirika la Habari nchini Tanzania, TBC ,kaimu katibu mtendaji wa BASATA, Onesmo Mabuye, alisema ''msanii au kikundi chochote kinachotoka nje ya nchi kwa ajili ya maonyesho lazima kipate kibali cha BASATA ili ikaonyeshe kazi kule inakokwenda katika weledi ambao sisi tunaufahamu na tunafahamu habari ya ratiba ile ya kwenda nje ya nchi , si hivyo tu akimaliza shughuli zake kula nje anaporudi nchini anapaswa kurudisha taarifa BASATA''.
BASATA inasema kuwa msanii huyu 'hakuona kama jambo hilo ni muhimu' pamoja na kushughulikia safari yake alisahau kipengele hicho ambacho kina umuhimu wake.
Kumekuwa na maoni mbalimbali kutoka kwa mashabiki wa muziki nchini Tanzania,hasa wakihoji kuhusu kanuni hii mpya ina umuhimu gani kwa wasanii?
Baraza la sanaa la taifa liliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuondoa sintofahamu hiyo ambayo ilionekana kana kwamba ni usumbufu kwa wasanii wanapokuwa katika utekelezaji wa kazi zao.
Gazeti la mwananchi nchini Tanzania lilimnukuu Meneja wa mwanamuziki huyo, Babu Tale akisema Diamond alitakiwa kuondoka Alhimisi mwendo wa saa 3.00 asubuhi lakini baada ya kuzuiliwa ilibidi aondoke saa 11.00 jioni baada ya kukamilisha taratibu za kupata kibali hicho.
"Ni kweli jana msanii wangu (Diamond) alikumbana na mkono wa Basata akiwa uwanja wa ndege. Kwa kuwa tulishalipwa hela ya watu ikabidi tukishughulikie kibali haraka ili aweze kuondoka nchini,"alisema.
Hata hivyo, alilaumu Basata kwa kushindwa kuweka wazi kanuni zake ili wasanii wazijue badala ya kuwasubiri wakosee ili wawachukulie hatua.
Baadhi ya kanuni mpya za BASATA mwaka 2018
- Vyombo vya habari havitaruhusiwa kupokea wala kurusha kazi za sanaa ambazo hazitakuwa na ithibati ya maadili kutoka Baraza
- Baraza litatoa ithibati ya maadili ya sanaa kwa maandishi na kupigwa muhuri wa Baraza kwa kazi za sanaa zilizothibitishwa
- Hakuna kazi ya sanaa itakayopelekwa sokoni ama kwa walaji bila kupewa kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui yamezingatia maadili
No comments:
Post a Comment