Zanzibar yapoteza uanachama wake CAF
Zanzibar yapoteza uanachama wake CAF.
Zanzibar imepokonywa uanachama wake katika Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) miezi minne baada ya kukubaliwa kuwa mwanachama.
Rais wa Caf Ahmad amesema Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haikufaa kukubaliwa kuwa mwanachama wa 55 wa shirikisho hilo mwezi Machi.
"Walipokelewa bila ya kufuatwa kwa sheria za shirikisho ambazo ziko wazi," amesema Ahmad.
"Caf haiwezi kukubalia uanachama wa mashirikisho mawili kutoka kwa taifa moja."
"Ufafanuzi wa maana ya taifa unatoka kwa Muungano wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa," amesema Ahmad katika mkutano mkuu wa kipekee wa shirikisho hilo nchini Morocco.
Fifa ilikataa kuipokea Zanzibar kama mwanachama hata baada ya hatua ya Caf, iliyoidhinishwa na mtangulizi wa Ahmad, Issa Hayatou.
Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini imekuwa ikiendesha shughuli zake za soka kivyake na kuwakilishwa katika mashindano ya soka ya kanda.
No comments:
Post a Comment