Hatimaye kiungo mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars Simon Msuva hatutamuona akicheza VPL kuanzia msimu ujao baada ya dili lake la kwenda kucheza nje kufikia pazuri
Muda wowote Msuva ataondoka kwenda Morocco kujiunga na klabu yake mpya Difaa Hassani El Jadidi (DHJ FC ) inayoshiriki ligi kuu nchini humo.
Dauda TV ilizungumza na Msuva ambaye yupo kwenye kambi ya timu ya taifa inayojiandaa kwa ajili mechi ya marudiano dhidi ya Rwanda kuwania kufuzu michuano ya CHAN 2018.
“Kila mtu anafahamu kwamba Simon amepata ofa na hili suala lipo mwishoni, kwa hiyo sasa hivi tunasubiri viza itoke ili watume tiketi niweze kwenda.
"Kwa upande wangu tayari nilishaongea na Yanga na wameshakubali na timu zote zimeshakubaliana, kwa hiyo kila kitu kipo mwishoni, ni kuomba Mungu tu,” alisema Simon Msuva.
Msuva anakwenda kuungana na Mtanzania mwingine Ramadhani Singano ‘Messi’ ambaye tayari ameondoka kwenda Morocco kujiunga na timu hiyo tangu Julai 14, 2017.
Difaa El Jadidi imemaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi msimu uliopita ikiwa na pointi 59 nyuma ya WCA Casablanca waliomaliza katika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 66. Ligi kuu ya Morocco inajumuisha timu 16 kama ilivyo kwa ligi kuu Tanzania bara (VPL).